Shirikisho La Vyama Vya Tiba Asilia Lampigania Dr.Mwaka Mahakamani

 SUMARIES
Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili Tanzania (Shivyatiata) linakusudia kwenda mahakamani kufungua kesi dhidi ya Baraza la Tiba za Asili likidai limewaadhibu kinyume cha sheria kwa kuwafungia matabibu saba na vituo vya tiba hiyo.

Mwenyekiti wa Shivyatiata, Abdulrahman Lutenga alisema jana kuwa Baraza hilo limewahukumu wenzao hao bila kuzingatia vifungu vya sheria namba 23 ya tiba za asili na tiba mbadala ya mwaka 2002, hivyo wameamua kwenda mahakamani kuomba tafsiri sahihi.

Lutenga alisema Shivyatiata imepokea barua za malalamiko kutoka kwa waganga walioadhibiwa na Baraza hilo, na baada ya kufanya uchunguzi wamebaini kwamba uamuzi huo ulitolewa bila kuzingatia taratibu na sera na uendelezaji wa viwanda katika eneo la tiba asili.

“Shivyatiata tunatambua kuwa Baraza hilo ni chombo cha kitaalamu kwa mujibu wa Sheria namba 23 ya tiba za asili na tiba mbadala hivyo lina mamlaka ya kuwaadhibu wanaokwenda kinyume cha sheria hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa onyo au kumsimamisha mganga au mkunga na muuzaji wa tiba za asili, lakini uamuzi uliochukuliwa na baraza hilo hatukubaliani nao,” alisema Lutenga. 

Alisema ingawa uamuzi unaweza kutolewa bila kikao kwa kuwapelekea wajumbe nakala za shauri, mjumbe yeyote anaweza kutaka uamuzi uahirishwe na suala hilo lijadiliwe katika kikao cha Baraza, lakini cha kushangaza mwenyekiti wa Baraza hakukizingatia kifungu hiki.

Alisema shirikisho hilo pia linamuomba Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutumia mamlaka aliyonayo kuwaondoa watendaji wa Baraza hilo kwa madai kuwa wamekuwa wakiwadhalilisha na kuwakatisha tamaa wanachama wake.

Katibu Mtendaji wa Shivyatiata Othman Shem alisema wameshangazwa na uamuzi wa Baraza hilo kwa kuwa waganga waliosimamishwa ni miongoni mwa waliokuwa wakiwategemea katika kuanzisha viwanda vya tiba za asili kutokana na uwezo wa kifedha na kitaalamu walionao.

“Baraza hili kweli linatakiwa kuajiri watu ambao wanataaluma hii kwa sababu mazingira ya uamuzi yanaonyesha umetolewa kwa lengo baya la kukandamiza taaluma yetu na kuturudisha nyuma kwa hatua tulizoanza kupiga,” alisema. 

Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk Edmund Kayombo alitangaza uamuzi kukifutia usajili kituo cha Foreplan kinachomilikiwa na Juma Mwaka kwa kutokidhi masharti ya usajili na kufanya kazi kinyume cha usajili wake.
Previous
Next Post »