Nice: ‘Nilimuona muuaji’, aliyeshuhudia asimulia

 Mmoja wa watu walioshuhudia dereva wa lori akiwakanyaga na kuwaua watu 84 mjini Nice, kusini mwa Ufaransa amesimulia yaliyojiri.
Nader el Shafei, raia wa Misri, alinusurika pembamba kuuawa.
Anasema lori lilisimama mita moja kutoka eneo alikokuwa.
Alipiga video dereva huyo akipigwa risasi na kuuawa na maafisa wa polisi.
“Ulikuwa muda mfupi baada ya fataki kulipuliwa, watu wote walikuwa ufukweni – nilikuwa miongoni mwao, nikisherehekea siku ya taifa ya Ufaransa.
“Dakika tano baada ya shrehe kumalizika, watu wote walikuwa wakitembea katikati mwa barabara tuliposikia vilio. Niliona lori likija kuelea eneo nilikokuwa.
 “Nilikuwa mbele ya lori katika barabara kuu na niliwaona watu wakiwa mvunguni mwa lori, wakiwa wamepondwa.
“Alisimama mbele yangu, mita moja hivi – nilimuona kupitia dirisha.
 “Mwanzoni, nilidhani kutoka kwa watu waliokuwepo kwamba ilikuwa ni ajali tu na kwamba alikuwa amepoteza udhibiti wa gari na akawagonga watu kimakosa.
“Kwa hivyo, nilikaa nikimwambia kwa sauti ya juu asimame, kwa sababu kulikuwa na watu chini ya lori. Lakini hakuwa anamwangalia yeyote – alikuwa tu anaendesha lori kwa njia ya wasiwasi na ukali, kana kwamba alikuwa anatafuta kitu.
“Mikono yake ilikuwa kwenye kidhibiti gari – nilidhani alikuwa amepoteza usukani na alikuwa anajaribu kulisimamisha lori.
“Lakini niliona anachukua kitu kutoka chini – kilionekana kama simu, kwa hivyo, tena, nikadhani labda anataka kuita ambiulensi.
“Ghafla, niliona polisi wanakuja kutoka nyuma yangu, kwa sababu nilikuwa namwamngalia tu. Na nikamuona anatoa bunduki yake, na kuanza kufyatua risasi kupitia dirishani.
“Wakati huo, polisi walinisukuma na kuniondoa, na kunihimiza nikimbie. Walikaa wakiniambia “degagez” [ondoka]. Kwa hivyo, nikarudi nyuma hatua nne hivi.
“Nilichukua simu yangu na nikaanza kupiga video ya ufyatulianaji risasi uliokuwa unaendelea.
“Sikukimbia – nilikuwa nimeganda. Nilipiga video ya kila kitu, hadi polisi walipomuua.
“Afisa wa polisi aliniona nikipiga video – akaja kwangu na kunifokea na kunitaka nikimbie. Nililala tu, kwa sababu walikuwa wanasema “laleni, laleni” kwa sababu ya risasi na ufyatuaji risasi uliokuwa unaendelea.
“Kwa hivyo, nililala chini, lakini bado niliendelea kupiga video. Na hapo tena (polisi yule) akanijia tena, moja kwa moja, akiniambia kwa sauti, pamoja na wengine tuliokwua ufukweni na kututaka tukimbie – Nafikiri labda alidhani kunaweza kuwa na bomu kwenye lori.
“Wakati huo, niligundua kwamba mambo yalikuwa mabaya, na nikaanza kukimbia na wengine ufukweni.”
Previous
Next Post »