Msako Wa Makonda Dar Wa kamata Ombaomba 60

Katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ombaomba 60 wamekamatwa katika msako unaoendelea.

 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Magembe amesema wamewakamata 60 na operesheni inaendelea.

“Ukamataji wa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam unaendelea, 60 wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka,”  amesema Dk Magembe.

Amesema miongoni mwa ombaomba hao, wapo watoto wenye umri wa chini ya miaka 18   ambao wamepelekwa katika vituo vya watoto yatima, kikiwamo Kituo cha Kurasini.

Dk Magembe amesema  bado ombaomba wamekuwa wakionekana jijini  Dar es Salaam kutokana na kuwapo kwa watu wanaotoka mikoani na kuingia katika makundi ya ombaomba kila siku.

Amesema  uongozi wa mkoa unashirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoa elimu mikoani kuhusu operesheni ya kuwaondoa ombaomba.

Amesema ombaomba wengi wanakuja kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Awali  Makonda alitangaza operesheni kubwa ya kuondoa ombaomba katika Jiji la Dar es Salaam.

aliwataka polisi kwa kushirikiana na ustawi wa jamii kuwaondoa ombaomba wote waliopo mitaani.

Pia, Makonda amepiga marufuku wananchi wanaowapa fedha ombaomba  kuacha mara moja ili wajitafutie riziki wenyewe kwa kufanya biashara au kurudi mikoani kujishughulisha na kilimo.
Previous
Next Post »